Wasomi, wanasiasa waichambua CCM
WASOMI na wanasiasa nchini wameunga mkono agizo lililotolewa na
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli, lililowataka viongozi wa
Serikali kuwajibika mbele ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
iliyotolewa juzi wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho, mjini Dodoma.
Wakizungumza na gazeti hili, wasomi hao akiwemo Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana, alisema agizo hilo siyo
jipya isipokuwalimekuwa halitekelezwi kutokana na kutukuwepo kwa
msisitizo uliowekwa tangu nyuma katika masuala hayo ya uongozi.
Alisema kutokana na uwepo wa Ilani na sera zinazosimamiwa na kila
chama, hakuna ubishi kwa serikali iliyowekwa madarakani na chama
chochote cha siasa, kutekeleza kile kilichopo ndani ya sera kulingana na
utaratibu huo uliowekwa, na kwamba agizo hilo la Rais Magufuli
limelenga kuwakumbusha viongozi hao wa serikali.
“Ni kauli ya Rais, yeye pia ndiye Mwenyekiti wa Taifa wa chama na
msimamizi namba moja wa Ilani na sera za chama, alichokisema hakina
ubishi kuwa ndicho kinachopaswa kutekelezwa na viongozi wa serikali kwa
kuwa ndiyo wenye Ilani inayotekelezwa na serikali kwa sasa,” alisema Dk
Banna.
Alisema utendaji huongozwa na kusimamiwa na mambo mawili ambayo ni
Katiba pamoja na Ilani ya chama, na kwamba ni suala lisilopingika pia
kuona sera ikibeba mambo yote yaliyopangwa kutekelezwa katika Ilani kwa
utaratibu ule ule uliowekwa na chama kilichopo madarakani.
Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk
Bashiru Ally alisema ni suala lililo wazi kuwa siasa na utendaji ni vitu
visivyoweza kutenganishwa, hivyo suala la msingi ni kwa watendaji wa
serikali kufuata utaratibu kwa lengo la kuepuka misuguano.
Akitolea mfano wa namna Bunge linavyoisimamia serikali, Dk Bashiru
alisema kama ilivyo kwa utendaji huo, vivyo hivyo watendaji wa serikali
wanapaswa kujua kuwa anayewaonesha njia ya utendaji wao ni mwanasiasa
huku wote wakiwajibika kwa bosi wao ambaye ni mwananchi.
“Hakuna ubishi kuwa wanasiasa ndiyo wanaoonesha njia huku watendaji
wakibaki kuwa wawajibikaji kwa kupenyeza utaalamu wao, hauwezi
kuwatenganisha, jambo la msingi ni wote kufanya kazi kwa kuheshimiana
ili kuepusha msuguano wa namna yoyote unaoweza kujitokeza,” alisema Dk
Bashiru.
Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na Mhadhiri wa vyuo mbalimbali
nchini, Profesa Mwesiga Baregu alisema licha ya kauli hiyo ya Rais
kupokewa vyema na wajumbe wa mkutano huo na baadhi ya wananchi, bado
kunahitajika ufafanuzi kwa kiasi fulani ili kuondoa misuguano baina ya
wanasiasa na watumishi wa umma.
Alisema anachoona hapo ni kuwa Ilani ya chama haiwezi ikazitangulia
sheria za serikali, ikiwemo taratibu wa utekelezaji wa sheria za
utumishi wa umma, ila kutokana na kuzoeleka kwa hali hiyo ni vyema
likajengewa utaratibu wa wazi utakaosaidia kuondoa migogoro baina ya
pande hizo mbili katika jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP),
Augustino Mrema alisema kauli hiyo ya Rais Magufuli inatekelezeka kwa
kuwa hakuna ubishi kuwa CCM ndicho chama kilichounda na kuisimamia
serikali iliyopo madarakani kwa sasa.
Alisema hata kama ingekuwa hivyo kwa chama kingine chochote, ni jambo
la kawaida kwa serikali kufuata na kutekeleza yale yote yaliyowekwa
ndani ya Ilani ya chama hicho na mengine ni kulingana na matakwa ya
chama husika ili mradi kama hayavunji utaratibu uliopo katika katiba ya
nchi.
Aidha Mrema alimpongeza Rais Magufuli kwa kudai kuwa uongozi wake
‘umetukuka’ ndani ya CCM na Tanzania kwa ujumla ndani ya muda mfupi
tangu aingie madarakani, kutokana na hatua yake ya kushughulikia masuala
mbalimbali yakiwemo ya ufisadi na mengineyo ndani na nje ya chama
chake.
Alisema CCM ya sasa kama ingekuwa ni mtu basi angesema ‘ameokoka’ kwa
namna ambavyo kila kitu ndani yake kimebadilika kuanzia utendaji hadi
uwajibikaji hivyo kutokana na hilo si jambo la kushangaza ‘upepo’ huo
ukaelekezwa pia kwa watumishi wa umma kuiga kilichopo CCM kwa sasa.
Comments
Post a Comment