MFANYAKAZI WA PPF AKAMATWA AKISAFIRISHA MIRUNGI
Polisi mkoani Kilimanjaro inamshikilia mfanyakazi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (PPF) kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alimtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Anitha Oswald (32).
“Askari wakiwa doria walimkamata Anitha Oswald, ambaye ni mkazi wa
Karanga, Manispaa ya Moshi, akiwa anasafirisha dawa za kulevya aina ya
mirungi kilo 216 na gramu 370 kwa kutumia gari lake analomiliki aina ya
Toyota Sienta rangi ya silva,” alisema kamanda Issah.
Kamanda Issah alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa eneo la Majengo kwa Mtei
Desemba 19 akitokea Njia Panda ya Himo kuchukua mzigo huo.
“Jeshi la polisi mkoani hapa liko makini, operesheni inaendelea na
hatutamvumilia mtu yeyote ambaye atabainika kujihusisha na biashara
hii”, alisema.
Kamanda huyo alisema polisi wanaendelea kumtafuta dereva wa gari hilo
ambaye alikimbia baada ya kulitelekeza lilipogonga mti wakati
akiwakimbia askari.
Comments
Post a Comment