SAKATA LA AIRTEL LAZIDI KUKOLEA....TEWUTA NAO WAIBUKA
Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa Mawasiliano
Tanzania (Tewuta) kimepongeza hatua ya Rais John Magufuli kumtaka Waziri
wa Fedha kuanza uchunguzi kubaini ukweli kuhusu ubinafsishwaji wa
Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).
Katibu Mkuu wa Tewuta, Junus Ndaro amesema chama hicho kinatambua fika
kuwepo mchezo mchafu uliosababishwa na Watanzania wachache wenye uchu wa
fedha wakisaidiana na wawekezaji kupora rasilimali hiyo ya Taifa.
Ndaro amesema leo Alhamisi Desemba 28,2017 kuwa, kwa muda mrefu chama
hicho kimekuwa kikitoa malalamiko kuhusu ufisadi huo serikalini lakini
hakikusikilizwa.
“Tunampongeza Rais Magufuli kwa kuthubutu kutamka pasipo shaka kuwa
taarifa alizonazo zinaonyesha kampuni ya Airtel ni mali ya TTCL, jambo
hili tulilipigia kelele kwa muda mrefu,” amesema.
Ndaro amesema mara zote hawakusita kutamka kuwa Celtel ambayo sasa ni Airtel ni mali ya TTCL iliyoporwa pasipo kulipwa chochote.
“Wafanyakazi tunatambua kuwa TTCL haikuporwa Celtel pekee bali
ilinyang’anywa pia Chuo cha Posta na Simu hali iliyosababisha tukose
mahali pa kupata mafunzo,” amesema Ndaro.
Kutokana na kuanza uchunguzi wa sakata hilo, Ndaro amesema viongozi wa
Tewuta wako tayari kutoa kila aina ya ushirikiano kuhakikisha Serikali
inashinda na kuirudisha Airtel mikononi mwa TTCL.
“Tuna ushahidi wa kutosha na tuko tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali
katika hatua zote kuleta haki iliyopotea ya Kampuni ya Simu Tanzania,”
amesema.
Comments
Post a Comment