Wanawake Dar walizwa mamilioni na wazungu kupitia Facebook
AHADI ya zawadi kubwa ikiwemo fedha na kutekwa kimapenzi kwa njia ya
mtandao, kumewaliza mamia ya wanawake wa Jiji la Dar es Salaam.
Watu hao wameingia katika wimbi la kutapeliwa mamilioni ya fedha na
‘wapenzi’ wao hao, wanaojitambulisha kuwa ni raia wa mataifa ya Ulaya na
Marekani. Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa muda wa zaidi ya
mwezi mmoja sasa, kwa kuzungumza na wanawake watano, umebaini kuwa mamia
ya wanawake wamelizwa kwa kutapeliwa fedha na wazungu hao,
wanaofahamiana nao katika mtandao wa Facebook, huku wakiponzwa na ahadi
za mapenzi na zawadi mbalimbali, ikiwemo fedha.
Matapeli hao huwafuatilia wanawake kwenye mitandao ya kijamii hasa
Facebook, ambapo huanza kwa kuwaomba urafiki na kisha kupeana namba za
simu na ndipo mwanzo wa mawasiliano ya kina yanapoanza.
Gazeti hili limebaini kuwa mtandao huo wa matapeli, hutumia namba
mbalimbali za simu katika kuwatapeli wanawake zikiwemo namba za Ulaya,
Marekani na za nchi jirani katika kuwasiliana na walengwa wao kwa njia
za ujumbe mfupi wa maneno, huku gia yao ya kwanza ikiwa ni kuomba
uhusiano wa kimapenzi.
Vyanzo vya kuaminika vilivyozungumza na gazeti hili, wakiwemo baadhi
ya wanawake ambao tayari wametapeliwa fedha nyingi, vilisema wazungu hao
baada ya kuomba urafiki na kukubaliwa, huendeleza mawasiliano kwa njia
ya ujumbe mfupi au mazungumzo na wahusika kwa kasi ili kuwaaminisha juu
ya uhusiano wao.
Wakati wote wa mawasiliano, wazungu hao hutoa ahadi mbalimbali kwa
wanawake huku wakiahidi kuwatumia zawadi mbalimbali kama simu za gharama
kubwa, kompyuta mpakato, Ipad na dola za Marekani kati ya 20,000 na
30,000, huku lengo lao mahususi ikiwa ni kuwatapeli.
Mmoja wa waathirika wa matukio hayo, mkazi wa Tabata jijini Dar es
Salaam aliyeomba jina lake kuhifadhiwa, akieleza namna alivyotapeliwa
alisema; “Huyu mzungu kwanza alionesha interest (nia) ya mapenzi kwangu.
Mwanamke huyo ambaye alisema aliishia kutapeliwa Sh 550,000, alisema
mzungu huyo aliyekuwa anawasiliana naye, alijitambulisha kwa jina la Don
Collin, raia wa Uingereza. “Kwanza aliniomba urafiki Facebook, kabla ya
kumkubalia nilimfuatilia kuona taarifa zake na nikaona kuna baadhi ya
marafiki zangu Facebook ni marafiki zake kwa hiyo nikaondoa shaka dhidi
yake.
“Niliamua kumkubalia urafiki kwani alionekana kuwa ni mtu wa
kuaminika kwani mwanzoni kabisa wakati wa mawasiliano yetu
alijitambulisha kuwa ni Mwanajeshi anayefanya kazi kwenye meli ya
Uingereza.
Alisema waliendelea na urafiki wao kwa kutumia simu na Facebook kwa
muda mrefu, kabla ya kuanza kumtongoza. Alisema hatua hiyo ilizidi
kumuongezea uaminifu zaidi na ni wakati huo mzungu huyo alimpa taarifa
alizoona ni njema kuwa anataka kumtumia zawadi ya viatu, pochi, simu na
fedha Dola za Marekani 25,000 (zaidi ya Sh milioni 50).
“Sauti yake ilikuwa ni ile ya mzungu kweli. Alikuwa akijitanabaisha
kuwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kifedha na alisisitiza kuwa lengo la
kunitumia zawadi na fedha hizo ni kuimarisha uhusiano wa mapenzi kwangu
ambao alikuwa tayari ameuonesha,” alisema.
Alisema ilifika siku ambapo Mzungu huyo alimpigia simu na kumueleza
kuwa rafiki yake ambaye ni Mwanadiplomasia, alikuwa na safari ya kuja
Dar es Salaam na alisema ni nafasi nzuri ya kunitumia zawadi zangu
alizosema kuwa angezifunga kwenye sanduku maalumu na kunitumia namba ya
siri ya kulifungua.
“Nilikaa nikisubiri hadi siku nilipopigiwa simu na mtu kwa namba ya
hapa nchini akijitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akinitaarifu kuwa kuna mtu amekamatwa
uwanjani hapo akiwa na mzigo wangu.
“Aliniambia kuwa walimkamata kwa vile alikuwa na mzigo ambao ulikuwa
haujalipiwa kodi na hivyo alisisitiza kuwa watamuachia endapo ningetuma
Sh 550,000. Kwanza nilifanya utafiti kwa kumtumia mdogo wangu kujua kama
KIA kuna mtu mwenye jina hilo na nikathibitishiwa kuwa yupo.
“Kwa vile akili yangu ilikuwa juu ya zile Dola za Marekani 25,000
niliona ni bora nitume fedha hiyo. Ingawa nilitia shaka kuwa masuala ya
kodi hushughulikiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) lakini nilipochunguza
namba ya usajili ya simu na jina nililopewa na ofisa wa KIA niliona
yanafanana, hivyo nilituma fedha hizo,” alisema.
Alisema hata hivyo, muda mfupi baadaye, mtu huyo wa KIA alipiga simu
na kumweleza kuwa wakati wanaukagua mzigo huo kwa mashine (scanner) ili
kuruhusu kutoka, wamebaini kuwa kuna kiasi kikubwa cha dola
zinazosafirishwa isivyo halali.
Alisema wakati wote simu hiyo ilikuwa inabadilishwa kutoka kwa ofisa
wa KIA na Mwanadiplomasia huyo ili kuzungumza naye. “Walisema wamegundua
kupitia Scanner kuwa ni kiasi kikubwa cha Dola ila wameshindwa kujua ni
kiasi gani kwa vile sanduku hilo limefungwa kwa namba maalumu.
“Waliniambia kwa vile kitendo hicho ni kinyume cha sheria kutokana na
sheria kuruhusu mtu kusafirisha dola za Marekani zisizozidi 10,000,
aliyenitumia, aliyekutwa nazo na mimi, tumefanya kosa la jinai na
tunatakiwa kukamatwa.
“Hata hivyo, walianza kunishawishi kutoa fedha nyingine ili wauachie
mzigo huo, lakini pia sisi pia tuwe huru. Niliomba kuzungumza na yule
mwanadiplomasia nikamwambia atoe hizo fedha ili mimi nimrudishie
baadaye, akasema hakuwa na fedha taslimu.
“Nikawasiliana na Collins kumwambia akasisitiza nitume fedha ili
kumaliza suala hilo, akisema fedha zilizopo kwenye sanduku ni nyingi
zaidi hivyo nisikubali kuruhusu suala hilo kuwa kubwa,” alisema mwanamke
huyo.
Hata hivyo, alisema wakati huo alianza kupata shaka kuwa huenda kuna
utapeli unafanyika; na ndipo alipoanza kufanya uchunguzi wa kina wa jina
la ofisa wa KIA na namba ya simu aliyotumia kutuma fedha na kubaini
kuwa jina lilikuwa limetofautiana kwa herufi moja ya mwanzo.
“Hapo ndipo nilipobaini kuwa nimetapeliwa na nikasitisha kutuma fedha
nyingine wakati huo nikihangaika huku na kule kuanzia Tigo ili kuomba
fedha hizo kuzuiwa bila kupata msaada wowote.
Hata hivyo, kupitia wanawake 10 niliozungumza nao, gazeti hili
limebaini kuwa wapo wanawake ambao baada ya kutakiwa kutuma fedha za
awali kwa kisingizio cha kulipa kodi waliendelea kubanwa ili kulipa
fedha zaidi kati ya Sh milioni tano na 10, wakitishiwa kuwa bila kufanya
hivyo watakamatwa na kufikishwa mahakamani.
Kwa vile katika uchunguzi wake, gazeti hili lilibaini kuwepo kwa
wanawake wengine jijini Dar es Salaam (majina tunayo), ambao
wametapeliwa kwa mtindo huo, lilifanya juhudi za kuwasiliana na maofisa
wa Kitengo cha Kukabiliana na Uhalifu kwa njia za Kimtandao cha Makao
Makuu ya Jeshi la Polisi na kuzungumza na ASP, Mwangasa Joshua ambaye ni
Msaidizi wa Mkuu wa Kitengo hicho.
Katika ufafanuzi wake, Mwangasa alisema kuwa kumekuwa na kesi za aina
hiyo na nyinginezo nyingi zikitokea mara kwa mara na kuwa matapeli hao
hubadilisha mbinu kila kukicha.
Alisema, kikosi hicho kimefanikisha kuwakamata matapeli wa aina hiyo
na kesi zimefikishwa mahakamani na zinaendelea kungojea hukumu na
kusisitiza kuwa kikubwa ambacho kinatakiwa kufuatwa na wananchi ni
kuacha tabia ya kutuma fedha kwa watu wasiowajua.
“Najua tuna wajibu wa kukabiliana na wizi huu wa mtandaoni ambao
umewaliza wanawake wengi nchini lakini, wahusika wenyewe nao wasikilize
ushauri tunaoutoa kila siku wa kuwa wawe makini katika kutuma fedha
mitandaoni hata kama wanatuma kwa wapenzi wao ni lazima wajiridhishe,”
alisema Mwangasa.
Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu
Mwakyanjala aliwataka wananchi kuwa makini dhidi ya wahalifu hao kwa
njia za mitandao hasa kwa kutowapatia mwanya wa kuwaibia.
Comments
Post a Comment