WAKAMATWA NA KILO 64 ZA DAWA ZA KULEVYA AINA YA HEROIN
Wawili
wa Dar es Salaam wamekamatwa eneo la Kilambo mkoani Mtwara lililopo
mpakani na nchi ya Msumbiji wakiwa na pakiti zenye uzito wa kilo 64 za
dawa za kulevya aina ya heroin.
Akizungumza na Mwananchi jana, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na
Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga alisema watuhumiwa
walikamatwa Desemba 7 wakiwa na dawa hizo zikitokea mkoani Pemba nchini
Msumbiji kuingizwa Tanzania.
Sianga alisema pakiti hizo zilifichwa kwenye gari na kila moja ilifungwa kwa ujazo wa kilo moja.
Alisema watuhumiwa walipokamatwa walipelekwa kwa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa ajili ya ukaguzi wa kina.
Sianga alisema utaratibu wa kisheria unafanyika ili kuwafikisha mahakamani.
Kwa mujibu wa marekebisho ya sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za
kulevya, mtu akikamatwa anasafirisha dawa hizo zaidi ya gramu 20 hapewi
dhamana na adhabu yake ni kifungo cha maisha iwapo atatiwa hatiani.
Sianga alisema DCEA imewadhibiti wafanyabiashara wa dawa za kulevya
ambao sasa wanaitumia Msumbiji kupitishia mizigo na baadaye kuiingiza
nchini.
Alisema wana taarifa kuwa wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya
wamekimbilia nchi za jirani na wataendelea kuwafuatilia kuhakikisha
haziingii nchini.
Kamishna huyo alisema juzi waliteketeza ekari nne za bangi eneo la Arumeru Magharibi mkoani Arusha.
Alisema mamlaka inaendelea kuwatafuta watuhumiwa wanaohusika na mashamba hayo.
Kamishna wa Sheria wa DCEA, Edwin Kakolaki alisema kwa mujibu wa kifungu
cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya
namba 5 ya mwaka 2015 kama ilivyofanyiwa marekebisho watuhumiwa
hawatapata dhamana.
Alisema iwapo watatiwa hatiani na Mahakama, adhabu ni kifungo cha maisha
na mali zao ikiwemo gari waliokuwa wakilitumia kusafirishia dawa za
kulevya zitataifishwa.
Kakolaki alisema washtakiwa wa bangi na mirungi kwa mujibu wa kifungu
cha 11(1) (b) cha sheria hiyo wakipatikana na hatia adhabu ni kifungo
cha miaka 30 jela na huwa hakuna faini au dhamana.
Februari 10, Rais John Magufuli alianza kuisuka Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kumteua Sianga.
Comments
Post a Comment