Vigogo wamiminika kurejesha fomu
IKIWA leo ndiyo siku ya mwisho kwa viongozi wa umma, kuwasilisha fomu
za kuonyesha rasilimali mbalimbali walizonazo katika Ofi si za
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, viongozi mbalimbali
wakiwemo mawaziri, wabunge na wakuu wa wilaya ‘wamemiminika’ katika Ofi
si za Sekretarieti hiyo Jijini Dar es Salaam kuwasilisha fomu hizo.
Miongoni mwa viongozi waliofika na kuwasilisha fomu zao ni Waziri wa
Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe; Mbunge wa
Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na Mbunge
wa Ubungo, Saed Kubenea.
Wengine ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema; Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi na Mbunge wa Morogoro Kusini, Prosper
Mbena. Akizungumza na waandishi wa habari, Kamishna wa Maadili,
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu Harold Nsekela
alisema kumekuwepo na mwitikio mkubwa wa viongozi mbalimbali wanaofika
katika ofisi hizo katika kanda zote na kuwasilisha fomu zao.
Alisema hatua hiyo imetokana na muda uliowekwa kufikia mwisho leo,
hatua aliyosema kuwa kwa kiasi fulani ndiyo imesababisha kuwepo mwitikio
huo mkubwa, tofauti na siku za nyuma.
“Viongozi wengi wamewasilisha fomu zao kupitia wawakilishi wao
waliowatuma, kiutaratibu siyo vibaya ila wakati mwingine kunaweza
kukajitokeza tatizo lolote ndani ya fomu ikizingatiwa kuwa ndani yake
ina kiapo cha mhusika wa fomu,” alisema Jaji Nsekela.
Aidha alisema kutokana na mwitikio huo mkubwa, ofisi yake imeamua
kufanya kazi hadi jioni siku ya jana ambayo ni nusu siku, kwa lengo la
kutoa muda wa kutosha kwa viongozi mbalimbali kwenda kuwasilisha fomu
zao kabla ya kufikia tamati yake hii leo.
Alisema ukiacha baadhi ya viongozi wa umma waliowasilisha fomu zao
katika Jiji la Dar es Salaam, pia kupitia ofisi zake katika Kanda saba
zilizopo mikoa ya Arusha, Mbeya, Tabora, Mtwara, Mwanza, Kibaha- Pwani
na Dodoma, pia zimeweza kupokea fomu kutoka kwa viongozi mbalimbali
hususani jana kwa ajili ya kukimbizana na muda uliobakia.
Rais John Magufuli juzi aliwasilisha fomu yake na kumwagiza
Mwenyekiti wa Sekretarieti hiyo ya maadili, kusimamia muda mwisho
uliowekwa na ofisi yake huku akiwaonya viongozi watakaokwepa kuwasilisha
fomu hizo.
“Mheshimiwa Jaji Nsekela ikifika tarehe 31 Desemba ambayo ni siku ya
mwisho kwa mujibu wa sheria, weka mstari na usipokee fomu nyingine,
halafu tuone sharia itafanyaje,” alisema Rais Magufuli akimwagiza Jaji
Nsekela.
Kwa upande wake, Jaji Nsekela alisema, “Viongozi hawaombwi kujaza
fomu hizi, kuna baadhi wanadhani labda kutuletea hilo tamko ni fadhila,
hapana, sharia ya nchi inahitaji hivyo na kuna sababu zake za msingi.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema
amekwishawasilisha tamko la viongozi wa umma kuhusu rasilmali na madeni
kwenye Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma tangu juzi (Alhamisi
Desemba 28, 2017).
Akizungumza na waandishi wa habari kijijini kwake Namahema ‘A’
wilayani Ruangwa mkoani Lindi jana jioni, Waziri Mkuu alisema fomu hizo
zilipokelewa juzi na amekwishapatiwa barua ya kupokea tamko hilo.

Comments
Post a Comment