Sadifa wa UVCCM nje kwa dhamana
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoa wa Dodoma jana ilimwachia kwa dhamana
aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi Taifa
(UVCCM), Sadifa Juma Hamis (35) anayekabiliwa na tuhuma za rushwa.
Sadifa alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Desemba 11, mwaka
huu na kukataliwa dhamana baada ya upande wa mashtaka kudai akiwa nje
kwa dhamana ataingilia uchaguzi wa UVCCM taifa uliokuwa ukiendelea
wakati huo na kuingilia uchunguzi uliokuwa ukifanywa na Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Akisoma shauri hilo jana la uamuzi mdogo kuhusu dhamana, Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Fovo
alisema vigezo ambavyo vilitolewa na wakili wa serikali havihusiani kwa
namna yoyote kuvuruga uchunguzi na kuingilia upelelezi kama ambavyo
walidai upande wa mashtaka.
Alisema mshitakiwa anaruhusiwa kudhaminiwa kwani ni haki Kikatiba
kutokana na kifungu namba 15 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Hakimu Fovo alisema mazingira ya kesi hiyo na vigezo
vilivyotolewa na wakili wa serikali ni tofauti kabisa hivyo haoni sababu
ya kumnyima dhamana mshtakiwa.
Alidai kuwa Kifungu cha 15 (i) (b) walichokitumia mawakili wa
serikali kwa kuzuia dhamana kwa mtuhumiwa hakimzuwii mtu yeyote kupewa
dhamana hivyo sababu za upande wa Jamhuri hazikuwa na mashiko.
Mshtakiwa aliachiliwa huru baada ya masharti ya dhamana aliyopewa
ambapo alitakiwa kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini fungu la
dhamana la Sh milioni moja kila moja. Mshtakiwa alitimiza masharti hayo
ya dhamana na kuachiwa huru hadi Januari 18, mwakani kesi yake
itakapotajwa tena.
Mshtakiwa huyo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Donge Zanzibar
alifikishwa mahakamani Desemba 11, mwaka huu akikabiliwa na mashtaka ya
rushwa. Awali, ilidaiwa na Wakili wa Serikali kutoka Takukuru, Biswaro
Biswaro kuwa katika kesi hiyo ya jinai namba 232 ya mwaka 2017,
mshitakiwa alitenda kosa hilo Desemba 9, mwaka huu akiwa nyumbani kwake
maeneo ya Kata ya Mnadani Manispaa ya Dodoma.
Alisema katika kosa la kwanza Sadifa anadaiwa kuwa akiwa nyumbani
kwake alitoa rushwa ya vinywaji kwa wajumbe ili wamchague mgombea wa
nafasi ya Makamu mwenyekiti wa UVCCM, Rashid Mohamed Rashid.
Biswaro alisema kosa la pili analokabiliwa nalo Sadifa ni kutoa ahadi
ya kuwalipia gharama za usafiri wajumbe hao kutoka Dodoma– Kagera kama
zawadi kwao baada ya kumpigia kura mgombea huyo.
Wakili huyo aliwataja wajumbe hao kuwa ni Kadogo Shabani, Abdallah
Hamimu, Octavian Andrea, Didas Zimbihile, Tasinta Nyamwiza, John
Lufunga, Mtwawafu Kantangayo, Haleluya Ivody, Deocres Kagunila, Emmanuel
Shitobelo, Happiness Rynyogote, Adolf Andrew, Adinani Musheruzi, Editha
Domisian na Hashim Abdallah.
Biswaro alisema mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kinyume na Sheria
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 kifungu cha
15(1) (b) na (2).
Comments
Post a Comment