Chadema yajitosa Singida Kaskazini
NI wazi kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho awali kilitoa tishio la kutosimamisha wagombea katika uchaguzi wa marudio katika majimbo matatu ambayo uchaguzi utafanyika mapema mwakani, kimebadili mawazo na kusimamisha mgombea katika moja ya majimbo hayo.
Uhakika wa chama hicho sasa kujitosa kupambana na wapinzani wao
wakuu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) umejidhihirisha kupitia orodha ya vyama
iliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kushiriki uchaguzi
katika Jimbo la Singida Kaskazini mkoani Singida.
Katika orodha hiyo, vyama sita vya siasa, kikiwemo cha Chadema,
vimepitishwa na NEC kushiriki kwenye uchaguzi mdogo wa jimbo hilo la
Singida Kaskazini uliopangwa kufanyika Januari 13, mwakani.
Hata hivyo, orodha nyingine iliyotangazwa na NEC kwa Jimbo la Longido
mkoani Arusha haijamjumuisha mgombea wa Chadema na ACT Wazalendo.
Uchaguzi huo pia utafanyika Januari 13, mwakani.
NEC imetangaza kuwa vyama tisa vya siasa katika jimbo hilo la Longido
mkoani Arusha ndivyo vilivyojitokeza katika kinyang’anyiro cha kuwania
ubunge katika jimbo hilo na kufanikiwa kukamilisha vigezo vya kuwania
ubunge, ikiwemo cha kuchukua fomu na kurudisha kwa wakati muafaka.
Katika hatua nyingine, vyama tisa vimejitokeza kuchukua fomu kwa
ajili ya kushiriki uchaguzi mdogo wa nafasi ya ubunge katika Jimbo la
Songea Mjini mkoani Ruvuma, huku pia kukiwa hakuna wagombea wa Chadema
na ACT Wazalendo.
Jimbo la Singida Kaskazini Kwa mujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi wa
Jimbo hilo, Rashid Mandoa, Chadema ambacho awali kilitangaza kususa
chaguzi zote ndogo nchini, hatimaye kimempitisha David Djumbe kutetea
bendera ya chama chao katika kinyang’anyiro hicho.
Mandoa alivitaja vyama vingine vya siasa ambavyo vimesimamisha
wagombea wao kuwa ni Chama cha AFP mgombea akiwa ni Omari Sombi maarufu
kama OMOSO na Chama cha Wananchi (CUF), mgombea akiwa ni Dalphina Mlewa.
Vyama vingine vya siasa na wagombea wao kwenye mabano ni pamoja na
CCM (Justin Monko), ADA-Tadea (Aloyce Nduguta) na CCK mgombea wake akiwa
ni Mchungaji Yohana Labisu.
Mandoa alisema kuwa licha ya Chama cha NRA na UMD kuchukua fomu,
vilishindwa kuingia kwenye mpambano kutokana na kukosa wadhamini huku
UPDP na UDP pia vikikosa kushiriki baada ya kushindwa kurejesha fomu za
wagombea wao kwa muda uliopangwa.
Mgombea wa CCM, Justin Monko aliahidi kutekeleza kwa vitendo Ilani ya
uchaguzi ya chama hicho kutokana na kuwa na uzoefu wa kutosha katika
nyanja ya utendaji. “Rais wangu Magufuli aliponiteua kuwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri (DED) imekuwa kama vile kunipeleka kwenye
mafunzo.
Sasa nimeiva barabara na nawaahidi wananchi wangu utumishi uliotukuka
iwapo watanichagua,” alisema Monko. Hata hivyo, katika hali ya
kushangaza mgombea wa Chadema, Djumbe alitoweka ghafla ilipofika zamu
yake ya kuhojiwa na waandishi wa habari ili kujua sababu iliyomsukuma
yeye kugombea wakati msimamo wa chama chake ni kususa chaguzi zote ndogo
nchini.
Akizungumzia kuonekana kwa jina la Djumbe, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Vincent Mashinji alisema chama hicho kinazo taarifa za kutajwa kwa jina
la mgombea wake katika Jimbo la Singida Kaskazini lakini alisema ni
kutokana na kasoro zilizofanywa na NEC.
“Ni kweli mgombea wetu anasema amesikia Msimamizi wa Uchaguzi ametaja
jina lake na hivi tunavyozungumza amekwenda katika kituo cha uchaguzi
ili kuonana na msimamizi wa uchaguzi kujua sababu zilizomfanya ataje
jina lake bila jina lake kupitishwa na chama.
“Kwa kifupi ni kuwa msimamo wa chama chetu ni kutoshiriki uchaguzi
wowote wa marudio kama ilivyoamuriwa na Kamati Kuu,” alisema Mashinji.
Jimbo la Longido Akizungumza na waandishi wa habari jana baada ya muda
wa kurudisha fomu majira ya saa 10 kufika, Msimamizi wa Uchaguzi katika
Jimbo la Longido, Juma Mhina alisema kuwa vyama hivyo tisa vyote
vimekidhi vigezo na vimeruhusiwa kuanza kampeni kuanzia jana kwa kufuata
ratiba iliyopangwa na NEC katika jimbo hilo na si vinginevyo.
Mhina ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido
aliwataja wagombea na vyama hivyo kuwa ni pamoja na mgombea wa CCM, Dk
Steven Kiruswa. Wengine na vyama vyao kwenye mabano ni Kisiyongo Ole
Kunda (CUF), Francis Ringo (CCK), Feruzily Feruzilyson (NRA), Simon
Ngilisho (Chama cha Demokrasia Makini- CDM), Godwin Sarakikya (TADEA),
Simon Bayo (SAU), Mgina Mustafa (AFP) na Robert Laizer (TLP).
Msimamizi huyo alisema kuwa vyama vyote vilikaa jana kuunda kamati ya
maadili kwa ajili ya wagombea wenye kukiuka kanuni na sheria ya
uchaguzi, hivyo aliwaasa wagombea wote kuzingatia sheria za tume ya
uchaguzi katika mikutano yao ya kampeni na kufuata ratiba iliyopangwa.
Mhina alisema katika Jimbo la Longido lina kata 18 na vituo 175 vya
kupiga kura na waliojiandika kupiga kura katika jimbo hilo ni wananchi
57,808 na kampeni zimeanza jana na uchaguzi unaratajia kufanyika Januari
13, mwakani.
Katika urejeshaji fomu kulikuwa na shamra shamra mbali ambapo mgombea
wa CCM, Dk Kiruswa aliyesindikizwa na mamia ya wanachama wa mji wa
Longido aliwataka wanachama wa chama hicho kufanya kampeni kwa ustarabu,
hekima na busara kwa kunadi sera za chama na kusema yale mazuri
yanayofanywa na Rais Magufuli.
Dk Kiruswa alisema pia ni wakati wa wana CCM kuungana na kuondoa
tofauti zao na kuwashawishi wale wote waliokwenda upinzani kwa kufuata
mkumbo. Alisema na kuwataka wana CCM kuhudhuria uzinduzi wa kampeni
utakaofanyika Desemba 23, mwaka huu katika uwanja wa mpira uliopo karibu
na Kituo Kikuu cha Polisi cha mji wa Longido bila kukosa.
Naye Mgombea wa NRA Feruziyson alisema kuwa vyama vilivyosusa
uchaguzi katika jimbo hilo vinaogopa mageuzi na waoga katika demokrasia.
Alisema kususa uchaguzi ni kufanya wananchi kutowaamini na kushindwa
kuwapa dola hivyo kwa uamuzi uliofanywa na vyama hivyo umetia doa
upinzania.
Mgombea wa Demokrasia Makini, Ngilisho yeye alisema chama chake
kimejitoa na kushiriki uchaguzi huo kwa lengo la kuonesha kuwa chama
hicho kina watu makini wenye kujua demokrasi ni nini.
Ngilisho alisema kamwe chama hicho hakitasusa uchaguzi wa aina yoyote
kwani ni chama kinachojitambua na kujua nini maana ya upinzani na
kutaka kujitangaza zaidi vijijini kuliko mijini kama baadhi ya vyama
vingine.
Jimbo la Songea Mjini Kwa upande wa Jimbo la Songea Mjini, vyama tisa
vimejitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kushiriki uchaguzi mdogo wa
nafasi ya ubunge katika jimbo hilo. Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo,
Tina Sekambo alivitaja vyama ambavyo hadi jana tayari vilikuwa
vimeshajitokeza kuchukua fomu kuwa ni CCM, UPDP, Demokrasia Makini, AFP,
TLP, CCK, NRA, ADA na TADEA.
Comments
Post a Comment